Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kwa mnasaba wa “Sikukuu ya Muqawama na Ukombozi”, Sheikh Ahmad Al-Qattan, rais wa Jumuiya ya “Qawluna wal-‘Amal”, alipokea ujumbe wa “Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu” wa Lebanon katika ofisi yake iliyopo eneo la Barr Elias, Beqaa, ujumbe huo ulikuwa ukimjumuisha Sheikh Hussein Ghubris, mjumbe wa bodi ya uongozi, Sheikh Maher Mazhar na Sheikh Muhammad Al-Lababidi. Wajumbe hao katika mkutano huo, sambamba na kumpongeza Sheikh Al-Qattan kwa mnasaba huo, walisisitiza kushikamana na misingi ya Kiislamu na kitaifa.
Sheikh Al-Qattan katika mapokezi ya ujumbe wa "Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu" alisisitiza kuwa; Jumuiya ya “Qawluna wal-‘Amal” itaendelea kubaki mstari wa mbele katika mhimili wa muqawama na itasimama imara mbele ya miradi inayolenga eneo hili.
Akisisitiza kwamba: Sikukuu ya Muqawama na Ukombozi ni sikukuu ya kitaifa na ya kipekee inayotambuliwa rasmi na taifa la Lebanon na inayowakilisha mafanikio ya kihistoria ya kuwafukuza wavamizi kutoka ardhi ya Lebanon mwaka 2000, alitoa wito wa kuimarishwa kwa tukio hili kama nembo ya pamoja kwa Walebanon wote.
Sheikh Al-Qattan pia alieleza kwamba; nguvu ya Lebanon inatokana na umoja wa wananchi wake na kukusanyika kwao kuzunguka muungano wa jeshi, taifa na muqawama, na akaitaja kanuni hii kuwa ndiyo sababu ya kuilinda nchi na heshima ya wananchi wake.
Aidha, aliwapongeza wapiganaji wanaoitetea Lebanon nzima na kutoa wito wa kuimarishwa kwa umoja wa ndani mbele ya changamoto zilizopo.
Kwa upande mwingine, Sheikh Ghubris alisisitiza kwamba: “Sikukuu ya Muqawama na Ukombozi” inabeba maana za heshima, ushindi na utukufu, na ni fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio ya kihistoria yaliyopatikana.
Alisifu misimamo thabiti ya Sheikh Al-Qattan katika kusimama pamoja na wanyonge na chaguo la muqawama, na huku akionesha mshikamano wake naye, alisisitiza kuwa; kwa muda mrefu ameifahamu njia ya Al-Qattan inayojengwa juu ya kuwasaidia mafakiri na wanyonge pamoja na kusimama upande wa haki.
Ghubris akimwelekea Sheikh Al-Qattan alisema: “Mashambulizi na ukosoaji unaokuelekezwa hautakuzuia katika njia yako, tunakuhitaji uwe na subira na uthabiti, mashambulizi haya si tu kwamba hayapunguzi nafasi yako, bali yanaimarisha uwepo wako.”
Pia alisisitiza kwamba; Sheikh Al-Qattan anaungwa mkono kwa upana katika duru zinazounga mkono chaguo la muqawama, na akasisitiza kuendelea kusimama pamoja naye na kumuunga mkono mbele ya juhudi zozote za kuupiga mhimili huu.
Mwisho wa mkutano huo, ilisisitizwa umuhimu wa kuhifadhi umoja wa safu ya ndani na kuimarisha mshikamano kati ya nguvu za kidini na kitaifa; jambo ambalo kwa mujibu wa waliohudhuria linaimarisha chaguo la muqawama na kuilinda medani ya Lebanon mbele ya changamoto za sasa.
Maoni yako